Deuteronomy 9:6-29

6 aBasi mjue, si kwa sababu ya haki yenu Bwana Mungu wenu anawapa nchi hii nzuri kuimiliki, kwa kuwa ninyi ni taifa lenye shingo ngumu.

Ndama Ya Dhahabu

7 bKumbukeni hili, kamwe msisahau jinsi mlivyomkasirisha Bwana Mungu wenu kwa hasira huko jangwani. Tangu siku mlipotoka Misri mpaka mlipofika hapa, mmekuwa waasi dhidi ya Bwana. 8 cKule Horebu mliamsha ghadhabu ya Bwana, kwa hiyo alikasirika vya kutosha hata akataka kuwaangamiza. 9 dNilipopanda mlimani kupokea mbao za mawe, mbao za Agano lile Bwana alilofanya nanyi, nilikaa mlimani siku arobaini usiku na mchana, sikula mkate wala sikunywa maji. 10 eBwana alinipa mbao mbili za mawe zilizoandikwa kwa kidole cha Mungu. Juu ya mbao hizo kulikuwepo amri zote ambazo Bwana aliwatangazia kule mlimani kwa njia ya moto, siku ya kusanyiko.

11 fMwisho wa siku arobaini usiku na mchana, Bwana alinipa mbao mbili za mawe, mbao za Agano. 12 gKisha Bwana akaniambia, “Shuka chini mara moja, kwa sababu watu wako ambao umewatoa katika nchi ya Misri wamepotoka. Wamegeukia mbali haraka kutoka lile nililowaagiza, wamejitengenezea sanamu ya kusubu.”

13 hNaye Bwana akaniambia, “Nimewaona watu hawa nao ni watu wenye shingo ngumu sana! 14 iNiache, ili nipate kuwaangamiza na kufuta jina lao kutoka chini ya mbingu. Nami nitakufanya kuwa taifa lenye nguvu zaidi na kuwa wengi kuliko wao.”

15 jKwa hiyo niligeuka na kuteremka kutoka mlimani kwani mlima ulikuwa ukiwaka moto. Pia vibao vile viwili vya Agano vilikuwa mikononi mwangu. 16 kNilipotazama, niliona kuwa mmefanya dhambi dhidi ya Bwana Mungu wenu; mmejifanyia sanamu ya kusubu katika umbo la ndama. Mmegeuka upesi kutoka njia ile Bwana aliyowaagiza. 17 lKwa hiyo nilichukua vibao vile viwili nikavitupa na kuvipasua vipande vipande mbele ya macho yenu.

18 mNdipo tena nikasujudu mbele za Bwana kwa siku arobaini usiku na mchana. Sikula mkate wala sikunywa maji, kwa sababu ya dhambi yote mliyoifanya, mkifanya lile lililo ovu mbele za Bwana na kumkasirisha. 19 nNiliogopa hasira na ghadhabu ya Bwana, kwa kuwa aliwakasirikia vya kutosha na kutaka kuwaangamiza. Lakini Bwana alinisikiliza tena. 20Bali yeye alimkasirikia Aroni kiasi cha kutaka kumwangamiza, nami wakati huo nilimwombea Aroni pia. 21 oKisha nikachukua ile sanamu ya ndama mliyoitengeneza na kuichoma kwenye moto. Nikaiponda na kuisaga ikawa unga laini kama vumbi, nikatupa lile vumbi kwenye kijito kilichotiririka toka mlimani.

22 pPia mlimkasirisha Bwana huko Tabera, Masa na Kibroth-Hataava.

23 qVilevile wakati Bwana alipowatuma kutoka Kadesh-Barnea, alisema, “Kweeni, mkaimiliki nchi ambayo nimewapa.” Lakini mliasi dhidi ya agizo la Bwana Mungu wenu. Hamkumtegemea wala kumtii. 24 rMmekuwa waasi dhidi ya Bwana tangu nilipowajua ninyi.

25 sNilianguka kifudifudi mbele za Bwana kwa zile siku arobaini usiku na mchana kwa sababu Bwana alikuwa amesema angewaangamiza ninyi. 26 tNilimwomba Bwana na kusema, “Ee Bwana Mwenyezi, usiangamize watu wako, urithi wako mwenyewe ule ulioukomboa kwa uweza wako mkuu na kuwatoa katika nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu. 27 uWakumbuke watumishi wako Abrahamu, Isaki na Yakobo. Usiangalie ukaidi wa watu hawa, uovu wao wala dhambi yao. 28 vWatu wa nchi ile uliyotutoa sisi wasije wakasema, ‘Ni kwa sababu Bwana hakuweza kuwachukua mpaka nchi aliyokuwa amewaahidia, kwa sababu aliwachukia, akawaleta ili aje kuwaua jangwani.’ 29 wBali wao ni watu wako, urithi wako ule ulioutoa Misri kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyooka.”

Copyright information for SwhNEN